Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara zitakazofanyika katika uwanja wa Uhuru siku ya Ijumaa.

Tanzania itaadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Ijumaa wiki hii.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema kuwa sherehe zinazotarajiwa kufanyika siku hiyo ya kilele ya sherehe hizo ni gwaride la heshima lililoandaliwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama, maonesho ya Kikosi cha Makomandoo pamoja na gwaride la kimya kimya, burudani za vikundi vya ngoma za asili za mikoa ya Mbeya, Pwani, Lindi na kimoja kutoka Zanzibar.

Alizitaja shughuli nyingine kuwa ni kuimbwa wimbo maalumu ulioandaliwa na kwaya iliyoundwa na muungano wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama (Polisi, Magereza, JKT na JWTZ) na burudani kutoka bendi ya muziki wa kizazi kipya na kizazi cha zamani zitakazotumbuiza siku hiyo.

Itakuwa mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuwa mgeni rasmi katika shughuli ya maadhimisho ya sherehe za Uhuru, zinazofanyika kila mwaka Desemba 9, kwa kuwa mwaka jana aliziahirisha na kuagiza fedha takriban Sh bilioni 4.3 zitumike kupanua Barabara ya Morocco – Mwenge jijini Dar es Salaam.

Kaulimbiu ya sherehe za kutimiza miaka 55 ya Uhuru ni “Tuunge mkono jitihada za kupinga rushwa na ufisadi na tuimarishe uchumi wa viwanda kwa maendeleo yetu.”

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *