Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kufanya ziara ya siku tatu nchini Uganda.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda imesema Rais Magufuli atawasili nchini humo Novemba 9, 2017 na atapokewa na mwenyeji wake, Rais Yoweri Museveni.
Akiwa nchini humo pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli atashuhudia utiaji saini wa makubaliano mbalimbali.
Pia, atatembelea eneo litakalokuwa kituo cha pamoja cha huduma kati ya Tanzania na Uganda.
Taarifa hiyo imesema Rais Magufuli na mwenyeji wake watazungumza na waandishi wa habari Novemba 10,2017.
Ziara ya Rais Magufuli inafanyika katika wakati ambapo uhusiano wa mataifa hayo mawili ukitajwa kuimarika zaidi ikiwemo kuzinduliwa mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirishia mafuta.
Bomba hilo la mafuta ambalo litagharimu Dola 3.5 bilioni za Marekani litapita katika mikoa minane nchini.
Mara ya mwisho Rais Magufuli kutembelea Uganda ilikuwa Mei 2016 alipokwenda kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rais Museveni.
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amezitembelea nchi za Kenya, Rwanda na Uganda.