Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kesho anatarajia kupokea ripoti ya kamati ya pili ya wachumi na wanasheria iliyochunguza madini yaliyopo kwenye makontena yenye mchanga wa madini (makinikia).
Rais Magufuli atakabidhiwa ripoti hiyo Ikulu, Dar es Salaam ambapo tukio hilo litarushwa hewani moja kwa moja kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya redio, televisheni, mitandao ya kijamii na tovuti rasmi ya Ikulu kuanzia saa 3:30 asubuhi.
Mei 24, Rais Magufuli alipokea ripoti ya kamati ya kwanza yenye wajumbe wanane waliobobea katika fani za jiolojia, kemia, uhandisi kemikali na uhandishi uchejuaji madini, wakiongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma iliyochunguza aina na viwango vya madini yaliyomo kwenye mchanga wa madini uliomo ndani ya makontena yaliyokuwa yamezuiliwa bandarini na Serikali yasisafirishwe kwenda nje ya nchi.
Baada ya kupokea ripoti hiyo iliyoonesha mchanga uliokuwa unachunguzwa ulikuwa na wastani wa kiasi cha thamani kati ya Sh bilioni 829.4 kwa kutumia viwango vya wastani wa chini na trilioni 1.439 kwa kutumia viwango vya juu.
Kutokana na taarifa hiyo Rais Magufuli aliivunja Bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo kutokana na kutosimamia ipasavyo mchakato mzima wa usafirishaji mchanga wenye madini nje ya nchi na hivyo kuisababishia nchi hasara kubwa.
Aidha mbali na kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati, Profesa Sospeter Muhongo kuvunja Bodi ya TMAA na kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wake, Rais Magufuli pia aliviagiza vyombo vya dola kuwachunguza na kuwachukulia hatua watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na wengine waliohusika na kushindwa kusimamia vema mchakato mzima wa usafirishaji wa mchanga wenye madini nje ya nchi.