Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amesema kitendo cha kampuni kadhaa za uchimbaji madini kushirikiana na baadhi ya watumishi wa umma nchini kufanikisha utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi na kuwaacha Watanzania wakifa na kuteseka kwa umaskini, ni unyama usiovumilika na umefika mwisho.

Amesema hata kitendo cha taasisi za umma kuwabana wafanyabishara wadogo kwa kushindwa kujisajili na kulipa kodi huku taasisi hizo zikishindwa kuyabana makampuni yanayoingiza faida za mabilioni huku yakiwa hayajasajiliwa, ni unyama uliokithiri.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana baada ya kupokea ripoti ya Kamati maalumu ya kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na mchanga wa madini unaosafirishwa nje ya nchi iliyobainisha kuwa, kupitia mikataba michafu, Tanzania imepoteza takriban shilingi trilioni 108 katika kipindi cha miaka 19 toka mwaka 1998 hadi 2017 kupitia usafirishaji wa makinikia maarufu mchanga wa dhahabu.

Kutokana na hali hiyo, Rais ametoa maagizo ya kutaka mawaziri wote wa nishati na madini waliohusika kuliingiza taifa katika mikataba iliyolingamiza taifa kiuchumi, wahojiwe popote walipo.

Mawaziri waliopata kuongoza Wizara ya Nishati na Madini kati ya mwaka 1998 na 2017 ni Nazir Karamagi, Daniel Yona, William Ngeleja na Profesa Sospeter Muhongo. Wanasheria wakuu wa Serikali katika kipindi hicho, ni pamoja na Andrew Chenge, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Bunge, Johnson Mwanyika, Jaji Fredreck Werema na George Masaju aliyepo madarakani.

Pia amesema hakuna mchanga kusafirishwa kwenda nje ya nchi huku akiitaka kampuni ya ACACIA iliyotajwa kufanya kazi bila usajili nchini, kujitokeza hadharani kutubu na kukubali kurejesha mali zilizokwepa kulipa, ili kuruhusu hatua nyingine za usajili kuanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *