Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amefungua barabara ya lami ya Iringa – Migoli – Fufu yenye urefu wa kilometa 189 na ambayo inaunganisha Mkoa wa Iringa na Mkoa wa Dodoma.
Barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya kuanzia Cape Town nchini Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri (The Great North Road) imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 207.457 ikiwa ni ufadhili wa benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa asilimia 65.9, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa asilimia 21.3 na Serikali ya Tanzania imetoa asilimia 12.8.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema kukamilika kwa barabara hiyo kumeondoa adha iliyowakumba wananchi kwa miaka mingi ambapo safari ya Iringa – Dodoma iliyochukua siku nzima ama siku kadhaa wakati wa mvua, sasa inachukua muda wa saa 2:30.
Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Masaharu Yoshida na Mwakilishi wa AfDB Bw. Jeremy Aguma wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa miradi inayofadhiliwa na taasisi zao, na wameahidi kukuza zaidi ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo itakayosaidia kukuza uchumi wa wananchi kama inavyoelekezwa katika dira ya maendeleo ya mwaka 2025.
Wabunge wa Mkoa wa Iringa wakiongozwa na Mbunge wa Ismani na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Vangimembe Lukuvi wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake zilizoyawezesha majimbo yao kupata miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara, vituo vya afya na zahanati, Maji, uwanja wa ndege wa Nduli, Umeme, ruzuku ya elimu na dawa.