Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewatoa wasiwasi wananchi kwa kusema wazi kwamba anatamani siku moja ifike naye aitwe mzee mstaafu wa taifa hilo kama alivyo Kikwete na wengine.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo wakati akifungua uchaguzi mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), maarufu kama NEC Taifa, mkoani Dodoma akiwakaribisha na kuwatambulisha wageni mbalimbali waliohudhuria mkutano huo wakiwemo Marais wastaafu.
Vipindi vya ukomo kwa sheria iliyopo kwa nafasi ya Rais ni miaka 10 , sheria inaruhusu kila baada ya miaka mitano kufanyika kwa uchaguzi mkuu ili kuwapa demokrasia wananchi kuweza kuchagua kiongozi anayefaa.
Mwezi Julai, 2017 kuliibuka mijadala mbalimbali katika mitandao ya kijamii kujadili kauli ya Rais mstaafu ya awamu ya pili Alhaj Ally Hassan Mwinyi, aliyoitoa katika Baraza la sikukuu ya Iddi aliyosema kama isingekuwa matakwa ya kikatiba angetegemea kuona Rais aliyepo madarakani John Pombe Magufuli akipewa nafasi ya kutawala bila kikomo.
Mkutano huo wa leo utakipatia viongozi wapya wa ngazi ya juu chama hicho ikiwemo Mwenyekiti taifa na Mwenyekiti baraza la mapinduzi Zanzibar.
Tayari Rais magufuli amethibitisha kuwa katibu mkuu wa chama hicho Abdulrahman Kinana ataendelea na nafasi yake.