Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewatoa hofu wanafunzi wanaosomea fani ya ualimu nchini kuwa ajira za ualimu zipo hivyo wasiwe na wasi wasi.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo katika Mkutano Mkuu wa Chama Cha Walimu nchini Tanzania (CWT) uliofanyika mkoani Dodoma.
Rais amesema kuwa serikali inatoa ajira kwa walimu na kudai awali walisitisha zoezi la kuajiri kutokana na uhakiki wa vyeti feki kwa madai ya kuwa waliogopa wasije kurudia kosa la kutoa ajira kwa watu ambao hana sifa hizo.
Amesema kuwa “Mwaka huu pekee tumeajiri walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati wapatao 3,462 walimu wengine wapatao elfu kumi na tano na mia moja thelathini na tano wakiwepo wa Sayansi wanatarajiwa kuajiriwa wakati wowote baada ya vyeti vyao kuhakikiwa, kwa hiyo kuna walimu wa masomo mbalimbali tunahakiki vyeti vyao ili tusiingie kwenye matatizo ambayo tuliyaona na baada ya kuhakiki vyeti vyao wataajiriwa”.
Aidha Rais Magufuli amewatoa wasiwasi walimu wanafunzi na kusema kuwa ajira zipo nyingi hivyo wakimaliza masomo yao watapata kazi bila tatizo.