Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amesema kuwa mkuu wa mkoa yoyote atakayeshindwa kupeleka wawekezaji kujenga viwanda katika mkoa wake hatomvumilia.
Amewataka wakuu wote wa mikoa kuiga mfano wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, ambaye amekaribisha wawekezaji wanaojenga viwanda vipya.
Agizo hilo alilitoa Mwanza jana alipokuwa akituhubia mkutano wa hadhara eneo la Nyakato wilayani Ilemela.
Alisema ingawa Tanzania ilikuwa na viwanda vingi, hivi sasa Watanzania wamebaki hawapati majibu vilikwenda wapi hali inayoifanya Serikali iamue kufanya kazi ya kuvifufua vya zamani na kujenga vipya.
Kabla ya kuhutubia mkutano huo Rais alizindua kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona kilichojengwa Nyakato. Leo anatarajiwa kuzindua viwanda vingine viwili.
Alisema amefurahishwa na ahadi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela na kwamba kila anapopita ndani ya mkoa huo, lazima huzindua kiwanda ama viwanda kwa vile wawekezaji wengi hukimbilia kuwekeza mkoani humo.
Alimweleza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, ajirekebisha na afanye kazi ya kufufua, kufunga na kuchukua viwanda visivyofanya kazi na awape watu wengine.