Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wote wa kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Kitongoji nchini mwake kufuatilia matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo kwa lengo la kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya fedha hizo.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mnadani na kuwajumuisha wananchi wa Katoro na Buseresere Mkoani Geita.

Katika agizo hilo Dkt. Magufuli amewaonya walimu ambao wameanza kufanya udanganyifu kwa kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi kuliko idadi halisi kwa lengo la kupata mgao mkubwa wa fedha za ruzuku na amesema Serikali itachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika kufanya hivyo.

Pamoja na agizo hilo, Rais Magufuli pia ametaka viongozi wa ngazi zote katika Mikoa kuhakikisha wana takwimu za idadi ya wanafunzi katika shule zote zilizopo katika maeneo yao ili kurahisisha ufuatiliaji wa fedha hizo na amesema kuwa kuanzia sasa ataanza kutembelea shule kwa kushitukiza na kwamba kiongozi atakayeonekana kutojua takwimu itakuwa ni uthibitisho kuwa hatoshi kuendelea na wadhifa alionao.

Rais Magufuli ambaye ametumia mkutano huo kueleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali yake ya Awamu ya Tano, kutekeleza ahadi yake ya kujenga Tanzania Mpya pia amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa kutembelea wananchi wanaowaongoza badala ya kukaa muda mwingi ofisini huku akisisitiza ofisi hizo kuwepo katika maeneo yenye shughuli husika.

Aidha, Dkt. Magufuli amekosoa utaratibu unaotumiwa na Halmashauri nyingi za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya kutumia mawakala katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri akisema mawakala hao wamekuwa wakitumia utaratibu huo kukusanya fedha nyingi na kisha kuwasilisha kiasi kidogo katika Halmashauri husika.

Rais Magufuli amemaliza ziara yake ya siku nne katika Mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita na yupo nyumbani kwake Chato Mkoani Geita kwa mapumziko mafupi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *