Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mbunge mstaafu wa Jimbo la Moshi mjini, Philemon Ndesamburo kilichotokea jana.
Katika salamu za rambirambi alizozitoa Rais Magufuli kwenda kwa wafiwa pamoja na viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa.
“Kwa masikitiko nimepokea taarifa za kifo cha Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Moshi Mjini, Mzee wangu Philemon Ndesamburo kilichotokea katika hospitali ya rufaa ya KCMC iliyoko Moshi Mkoani Kilimanjaro”.
“Namkumbuka Mzee Ndesamburo kwa hekima zake na uongozi wake uliozingatia siasa za kistaarabu” alisema Rais Magufuli
Aidha, Rais Magufuli amesema alifanya kazi na marehemu Philemon Ndesamburo wakati wote wakiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wakati wote walishirikiana, kutaniana huku akimkumbuka kwa namna ambavyo alitumia muda wake bungeni kupigania mambo yenye maslahi kwa wananchi wa jimbo lake la Moshi Mjini.
Pamoja na hayo, Dkt. Magufuli ameitaka familia ya marehemu Philemon Ndesamburo na wote waliguswa na msiba huo kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu walichonacho.