Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wiki moja kwa Mawaziri kufanyia kazi na changamoto na maoni yaliyotolewa na wafanyabiashara katika mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara ili kuweza kutatua kero zao.
Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa baraza hilo ametoa maagizo hayo wakati akihitimisha mkutano huo ambao wafanyabiashara na wawekezaji kutoka sekta mbalimbali wamepata nafasi ya kueleza maendeleo ya shughuli zao, changamoto zinazowakabili na mapendekezo ya kuimarisha biashara na uwekezaji hapa nchini.
Aidha, miongoni mwa changamoto zilizowezwa kuwasilishwa katika mkutano huo ni pamoja na utozaji wa kodi unaoathiri biashara na uwekezaji, urasimu wa taasisi za serikali, udhibiti wa bidhaa za kutoka nje ya nchi zinazoathiri uzalishaji wa bidhaa za ndani, uwepo wa sheria na kanuni kandamizi kwa biashara na uwekezaji na utendaji usioridhisha kwa baadhi ya maafisa wa Serikali.
Rais Magufuli amewataka Mawaziri kuandika maelezo yenye majibu ya changamoto na maoni hayo na kuwasilisha kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ndani ya kipindi cha wiki moja ili serikali ifanyie kazi na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini.
Kwa upande mwingine, Rais Magufuli ametoa wito kwa wafanyabiashara hao kuhakikisha wanashiriki katika miradi mikubwa anayotekelezwa na serikali ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima – Uganda hadi bandari ya Tanga – Tanzania, na amewataka wafanyabiashara wanaofanya vitendo vya udanganyifu katika kodi na uingizaji wa bidhaa wabadilike.