Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka benki kuu ya Tanzania (BoT) wawe wasimamizi wazuri wa fedha za nchi.
Rais Magufuli amesema hayo leo alipokuwa akizindua tawi moja la Benki mkoani Dodoma na kuzitaka benki zote pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuangalia suala la matumizi ya fedha za kigeni ndani ya nchi kwani jambo hilo linazidi kuuwa uchumi wa nchi.
Magufuli amesema kuwa “Haiwezekani nchi ikawa na ‘curency’ mbili, tatu au zaidi zinazotumika zinaharibu uchumi, haiwezekani mtu ukiwa na dollar unakwenda kununua bidhaa dukani, ukiwa na pounds unakwenda kununua chochote nchini huu si utaratibu wa uchumi. Na hili nikuombe Waziri, BoT na mabenki yote mlisimamie hili kikamilifu, na baya zaidi haya yamekuwa yakifanywa na BoT. Gavana upo hapa mnapotangaza tenda zenu hata za wafagiaji mnawalipa kwa Dollar “
Rais Magufuli aliendelea kuelezea “Sasa haiwezekani nyinyi BoT ambao mnasimamia fedha nyinyi hao hao mnakuwa wabaya wa kudhibiti fedha za nchi hili lazima muende nalo na mbadilishe haraka. Msije kuwa chanzo cha kuharibu uchumi wa nchi yetu. Najua mnanielewa nililizungumza jambo hili mara ya kwanza nimelirudia leo mara ya mwisho litakalotokea msije kunilaumu”.
Mbali na hilo Rais Magufuli amehitaji kuwe na uangalizi mzuri kwenye ‘Bureau de Change’ na kuwa na utaratibu ambao unaeleweka.