Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 3,319 katika maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Meja Jenerali Mstaafu Projest Rwegasira, imesema, wafungwa 585 wataachiwa huru kuanzia leo, huku wengine 2,734 wakipunguziwa kifungo na hivyo wataendelea kubaki gerezani hadi watakapomaliza sehemu ya kifungo kilichobaki.

Rais anatoa msamaha huo kwa mujibu wa ibara ya 45(1) (d) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Msamaha mwingine unahusu wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama vile ukimwi, kifua kikuu na saratani.

Jenerali Rwegasira amesema wafungwa hao ni lazima wathibitishwe na jopo la waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Mganga Mkuu wa Wilaya.

Kundi la tatu linahusu wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi. Jenerali Rwegasira amesema umri huo uthibitishwe na jopo la waganga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *