Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ametoa mchango wa Sh milioni tano kwa ajili ya kusaidia matibabu ya mtoto Haidari Bonge mwenye umri wa miaka saba anayesumbuliwa na tatizo la kuota nyama kichwani, mdomoni na machoni.
Mtoto huyo anayeishi Mbagala Kuu jijini Dar es Salaam, alianza kuota nyama miezi mitatu baada ya kuzaliwa na amekuwa akifanyiwa upasuaji wa kuondoa nyama hizo mara kwa mara.
Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo baada ya kutazama kipengele cha Hadubini “Habari kwa Kina” kilichorushwa hewani katika taarifa ya habari saa 2:00 usiku na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) juzi.
“Mimi na mke wangu tumeguswa na tatizo linalomkabili mtoto Haidari Bonge na tumeamua kuchangia Sh milioni tano kutoka kwenye mshahara kwa ajili ya matibabu yake,” amesema Rais Magufuli na kuongeza:
“Pia tunatoa pole kwake na kwa familia yake ambayo imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kuhakikisha anapatiwa matibabu kwa kipindi kirefu cha miaka saba sasa.” Kwa mujibu wa Ikulu, mchango huo ulitarajiwa kukabidhiwa jana.