Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amesema serikali yake ya Awamu ya Tano inataka kuona mambo yanafanyika na kutoa matokeo bila kupoteza muda na kwamba angependa wadau wa maendeleo hasa China iende na kasi hiyo.
Aliyasema hayo jana alipofanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Biashara wa China, Qian Keming ambapo viongozi hao walikubaliana kuharakisha miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano wa nchi hizo mbili ukiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kati.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alimueleza Qian kuwa Serikali yake inataka kuona mambo yakifanyika na kutoa matokeo bila kupoteza muda.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma na kuunganisha nchi za Rwanda na Burundi ambao Tanzania imetenga Sh trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi katika bajeti hii, Rais Magufuli aliitaka China ambayo imekubali kushiriki katika ujenzi iendane na kasi ya serikali yake.
Ameongeza kuwa mradi huo una manufaa makubwa kwa Tanzania na nchi nyingine nane zinazotegemea Bandari ya Dar es Salaam na kwamba kukamilika kwake kutatoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ambayo imedharia kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Kwa upande wake Naibu Waziri huyo wa Biashara wa China alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kukuza uchumi wa Tanzania na kupiga vita rushwa na kuahidi kuwa serikali ya China itaongeza msukumo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kati.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing, Makamu wa Rais wa Benki ya Exim ya China Sun Ping, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.