Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli leo amepokea taarifa ya maridhiano kati ya serikali ya Tanzania na Kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akiwasilisha taarifa hiyo kwa Rais Magufuli, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Paramagamba Aidan Kabudi amesema kuwa serikali na Barric wamefikia maridhiano mazuri na timu ya Barric iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake, John L. Thornton.
“Nadhani hata wao wameamini kuwa tuna uwezo mkubwa wa kuingia katika maridhiano na kufikia makubaliano makubwa, tofauti na ambavyo tungeazima wataalam wa nje kuja kufanya majadiliano hayo kwa niaba yetu, heshima yetu ingeshuka.
“Barric wamependekeza tutumie mfumo wa gawio la 50 kwa 50 ambao ni mfumo wa karne ya 21, jambo ambalo litakuwa na manufaa kwa taifa letu. Tunakupongeza Mhe. Rais kwa kuchukua hatua kulinda Rasilimali za nchi. Hatimaye hatua hizo zimeanza kuzaa matunda.
“Serikali itakuwa na umiliki wa madini mengine yatakayopatikana kwenye makinikia na wao kubaki na fedha, dhahabu na shaba. Kampuni ya Barrick imekubali kulipa kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 300 kwa ajili ya kukuza Uaminifu,”.