Wafanyabiashara na wawekezaji nchini wameeleza kero na changamoto wanazokutana nazo katika uendeshaji wa shughuli zao, huku wakibainisha kuwa zimekuwa zikirudisha nyuma dhamira ya Serikali katika kukuza sekta binafsi nchini.
Wametoa kauli hizo leo Jumatatu Machi 19, 2018 Ikulu Dar es Salaam katika mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara, huku hoja zao zikichukuliwa na mwenyekiti wa baraza hilo, Rais John Magufuli.
Kabla ya kuanza majadiliano hayo, Rais Magufuli amesema leo utafanyika mjadala wa kuleta mabadiliko ambapo kila mfanyabiashara atasimama na kueleza kero na changamoto zinazomkabili, zitapatiwa majibu na watendaji wa Serikali, wakiwemo mawaziri.
“Leo kuna watu kama 13 kutoka Tume ya Mipango, nataka tuzungumze leo kwa uwazi, mimi hata tungezungumza leo na kesho sawa tu tuendelee , nataka mseme kwa uwazi, dakika tatu kila mmoja atazungumza , nataka tu-solve problem sio kila mara tunakutana hapa tunajadili mambo yaleyale,”amesema Rais Magufuli.
Mfanyabiashara Mwita Gachuma kutoka Mwanza ndiye ameanza kufungua mjadala huo akitoa kero mbili ikiwamo tozo kubwa zinazotozwa nchini ikilinganishwa na nchi jirani kama Kenya.