Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amewataka wanafunzi wa elimu ya juu nchini kutogeuza vyuo kuwa maeneo ya kufanya siasa na badala yake wasome na kufanya utafiti.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana alipofanya ziara katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kilichopo mkoani Morogoro.
Msingi wa agizo hilo, ulitokana na mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho ambaye pia ni kiongozi wa serikali ya wanafunzi, Peter Masoi kumwomba Rais Magufuli awape namna bora ya ukosoaji ili taifa lisiwe na vijana wakaa kimya.
“Mheshimiwa Rais, wewe ni kati ya mifano mikubwa na mimi kama kijana naifuata na ninaamini wakati wa ujana wako haukuwa mkaaji kimya kama vijana ambao hivi sasa tupo.
“Vijana ambao tupo hivi sasa tunayaona mambo ambayo huwezi kukosoa tukiamini huo ndiyo uongozi bora, mimi nilikuwa naomba walau leo utupe ile ‘confidence’ ya kutoka hapa ili mradi tu tuwe na namna bora ya ukosoaji. Tusiwe na taifa ambalo lina vijana wakaa kimya, ambao wanaona mambo yanaharibika bila kusema,”alisema mwanafunzi huyo.