Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemtaka Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage kuwanyang’anya viwanda watu waliouziwa na kisha kuvitelekeza viwanda hivyo ili kuwapatia wawekezaji wanaoweza kuviendeleza.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo jana muda mfupi kabla ya kufungua kiwanda cha kuzalisha saruji cha Kilimanjaro kilichopo katika eneo la Maweni Mjini Tanga.
Magufuli amesema nchi nzima ina viwanda 197 vilivyotelekezwa baada ya kubinafsishwa takribani miaka 20 iliyopita, vikiwemo viwanda vilivyopo Mkoani Tanga lakini anashangaa kuona Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji havinyang’anyi licha ya kutoa maelekezo ya kufanya hivyo mara kadhaa.
Magufuli pia aliwaagiza Wakuu wa Mikoa yote nchini kufanya tathmini ya viwanda vyote vilivyobinafsishwa katika maeneo yao ili kubaini ambavyo havifanyi kazi na kutafuta wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuviendesha.
Kiwanda cha Saruji cha Kilimanjaro kina uwezo wa kuzalisha tani 300 za saruji kwa siku na kinatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 3,000 kwa siku mwaka ujao.
Baada ya kufungua kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro Rais aliweka jiwe la msingi la upanuzi wa kiwanda cha kusindika maziwa cha Tanga (Tanga Fresh) ambacho kinatarajia kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita 50,000 kwa siku hadi kufikia lita 120,000 hatua ambao inatarajiwa kuongeza idadi ya wafugaji kutoka 6,000 hadi 12,000.
Kiwanda hicho kinamilikiwa na vyama vya ushirika vya wafugaji 24 kwa asilimia 42 na mwekezaji kutoka Uholanzi kwa asilimia 58 na upanuzi unaofanywa utaongeza uwekezaji kutoka Shilingi Bilioni 12 hadi kufikia Shilingi Bilioni 26.5.