Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kumnyang’anya pasi ya kusafiria (passport) Mkandarasi anayeshughulikia Mradi wa Maji wa Ngapa hadi hapo atakapokamilisha mradi huo.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo alipokwenda kukagua mradi huo wa maji ambao hadi sasa umetumia miaka 6 kujengwa lakini bado haujakamilika.
Pia Rais Magufuli amempa miezi miwili mkandarasi huyo kuhakikisha mradi huo unakamili huku RC Zambi akiwa na jukumu la kuhakikisha kuwa mkandarasi hatoki eneo hilo la mradi.
Mradi huo unaotarajiwa kumaliza tatizo la maji mkoani Lindi umegharimu shilingi bilioni 29 ambapo hadi sasa mkandarasi amelipwa bilioni 21.
Rais Magufuli amesema kuwa kama tatizo ni fedha ndio sababu mradi haumaliziki aambiwe ili atoe fedha serikali kuu kukamilisha wananchi waweze kupata maji.
Rais Magufuli anatarajiwa kukamilisha ziara yake mkoani Lindi leo jioni ambapo ataanza safari ya kwenda mkoani Mtwara atapofanya ziara yake Jumamosi na Jumapili.