Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Mwanga kuwasaka, kuwaka mata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wafugaji wote waliohusika kuwashambulia kwa viboko wananchi wa Kijiji cha Fukayosi kilichopo Wilayani humo.
Magufuli aliyekuwa akisafiri kwa gari kutoka Dodoma kwenda Jijini Dar es Salaam ametoa agizo hilo jana aliposimama katika kijiji hicho baada ya kuona wananchi wengi wakiwa wamekusanyika kando ya Ofisi ya Kata.
Baada ya kusimamisha msafara wake, Rais Magufuli aliwaita wananchi waliokuwa wamekusanyika huku wakiwa wameshika mabango yaliyoandikwa ujumbe wa kutaka wafugaji wa jamii ya Wamang’ati waondolewe na kisha akatoa nafasi kwa baadhi yao kueleza dukuduku lao.
Wananchi hao ambao ni wakulima na mfugaji mmoja aliyejitokeza wakaeleza kuwa Wamang’ati wamekuwa wakiwanyanyasa kwa kuingiza mifugo katika mashamba yao ya mazao na wakithubutu kuwakataza wamekuwa wakichapwa viboko na baadhi kuuawa.
Pia Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Wilaya hiyo kukomesha mara moja vitendo vya wafugaji kuwapiga wakulima na wakulima kuwapiga wafugaji, na pia kukomesha vitendo vya wafugaji kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.