Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuachana na utaratibu wa kutoa zabuni za uendeshaji wa bandari kwa kampuni binafsi ambazo huingia mikataba isiyo na manufaa kwa nchi na kusababisha uwepo mianya ya upotevu wa fedha za umma.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo jana kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa gati namba 2 ya bandari ya Mtwara ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuchukua muda wa miezi 21 kuanzia sasa.
Mapema Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa alisema gati namba 2 itakayojengwa katika bandari ya Mtwara itakuwa na urefu wa mita 350 na ujenzi wake utagharimu Shilingi Bilioni 137.5 zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema imelazimu kuongeza gati katika bandari ya Mtwara baada ya kuwepo ongezeko la mizigo inayosafirishwa kupitia bandari hiyo ambapo kiwango cha mizigo inayohudumiwa kinatarajiwa kuongezeka kutoka tani 273,886 mwaka 2015/2016 hadi kufikia tani 388,000 mwaka 2016/2017 kiwango ambacho kinakaribia ukomo wa uwezo wa bandari hiyo yenye uwezo wa kuhudumia tani 400,000 kwa mwaka.