Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi la barabara za juu ‘Flyovers’ ubungo jijini Dar es Salaam.

Barabara hizo za juu za ngazi tatu (Interchange), itagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 188.71 na itajengwa kwa muda wa miaka 3 na kuhusisha barabara za Nelson Mandela na Sam Nujoma ambapo takribani magari elfu 60 ambayo yatatumia barabara hizo kwa siku na kuwa mwarobaini wa msongamano wa magari katika makutano ya eneo la Ubungo.

Rais Dkt. Magufuli amesema serikali yake inalenga kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji na kuchochea mapinduzi ya viwanda na kuweka wazi miradi mingi ya ujenzi wa barabara ambayo analenga kuijenga hivi karibuni na kuiweka Tanzania kwenye nchi ya uchumi wa kati.

Kwa upande wake Rais wa Benki ya Dunia Dkt .Jim Yong Kim amesema, hatua hii ni ya kupeleka faida kwa jamii na kuchochea maendeleo yao, na kwamba Benki hiyo haiungi mkono miradi ya kizembe akitolea mfano ubinafsishaji ambao uliwahi kuleta hasara kwa jamii lakini sasa wanawezesha serikali kwa kutelekeza vipaumbele vya maendeleo na kuahidi kushirikiana na serikali ya Tanzania.

Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amewataka wakandarasi waliopewa tenda ya kujenga barabara hizo kutoa kipaumbele kwa watanzania kupata ajira katika ujenzi wa mradi huo, wenye lengo la kurahisisha usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *