Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli jana amefungua barabara ya lami ya Kyaka – Bugene Mkoani Kagera yenye urefu wa kilometa 59.1 iliyogharimu Shilingi Bilioni 81.597 fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Kyaka – Bugene – Kasulo yenye urefu wa kilometa 183.1 ambayo inaiunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda na Burundi.
Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli amesafiri kwa barabara hiyo kutoka Kyaka hadi Karagwe zilipofanyika sherehe za ufunguzi na amempongeza mkandarasi, kampuni ya CHICO ya China, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na timu ya wataalamu wa TANROADS kwa kuusimamia mradi huo wao wenyewe kwa gharama ya shilingi Milioni 519.2 badala ya kuajiri msimamizi ambaye angelipwa zaidi Shilingi Bilioni 4.5.
Rais Magufuli pia amezungumza na waandishi wa habari waliokuwa wakirekodi na kurusha matangazo ya sherehe hizo ambapo amewashukuru kwa kazi kubwa wanayoifanya na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao, na ipo tayari kuwasaidia ikiwa ni pamoja na kuwezesha mafunzo ya kuwaongezea ujuzi.
Sherehe za ufunguzi wa barabara ya Kyaka – Bugene zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakiongozwa na Prof. Norman Sigalla King, Wabunge wa Mkoa wa Kagera na viongozi wa Dini na Siasa.
Akiwa njiani kuelekea Karagwe Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Kyaka na kusikiliza kero zao ambapo amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Kagera kutowabughudhi wananchi wanaojihusisha na shughuli za kilimo, na badala yake wawasaidie kuondoa migogoro ya ardhi, kusajili mifugo yao na kuinua uzalishaji wa mazao ili Mkoa wa Kagera uwe na malighafi za kutosha kuanzisha viwanda.