Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amesema katika kipindi cha mwaka mmoja alichoiongoza Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ameshindwa kutatua changamoto aliyoikuta ya wanachama kushindwa kusaini mkataba wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ulaya (EPA).
Magufuli alitoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wa 18 wa viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo ambao pamoja na mambo mengine alikabidhi uenyekiti kwa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.
Amesema masharti yaliyopo katika mkataba huo ni mengi na ana uhakika katika kipindi kinachoanza, watazungumza na EU ili waweze kurekebisha masuala ambayo yamewafanya washindwe kusaini.
Pia amesema changamoto nyingine aliyoshindwa kuitatua na inabidi iendelee kufanyiwa kazi, ni migogoro ya kisiasa iliyopo katika nchi za Sudan Kusini na Burundi.
Amewataka viongozi wanaovutana katika nchi hizo mbili kuweka masilahi ya mataifa yao mbele na kuacha kuangalia masilahi binafsi ili waweze kutatua migogoro ya kisiasa waliyonayo.
Amesema jumuiya hiyo ilifanya jitihada kuhakikisha inapunguza migogoro hiyo kwa kipindi alichokuwa mwenyekiti.
Pia alisema EAC katika kipindi cha mwaka mmoja imefanikiwa kubana matumizi kutoka Dola milioni 12.6 za Marekani hadi milioni 9.1.