Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameanza ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu nchini Uganda kwa mwaliko wa Rais Yoweri Museveni.

Rais Magufuli amewasili Mtukula mpakani mwa Tanzania na Uganda ambako amepokewa na mwenyeji wake Rais Museveni aliyeambatana na mkewe Janeth.

Katika mapokezi hayo leo Rais  Magufuli amepigiwa mizinga 21 na amekagua gwaride  lililoandaliwa kwa heshima yake.

Viongozi hao wawili watafungua kituo cha pamoja cha huduma za mpakani (One Stop Border Post – OSBP) kilichojengwa ili kurahisisha utaratibu wa forodha, uhamiaji na kuharakisha biashara kati ya nchini hizi mbili.

Taarifa ya Ikulu imesema baadaye leo, marais hao wataweka jiwe la msingi katika mradi wa bomba la mafuta ghafi linaloanzia Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Baada ya ufunguzi, viongozi hao watazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika  wilayani Kyotera nchini Uganda.

Rais Magufuli jioni ya leo atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Rais Museveni katika mji wa Masaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *