Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha utoaji wa leseni mpya za uchimbaji madini.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Geita ambao walizuia msafara wake katika maeneo mbalimbali wakati akiwa njiani kuelekea Chato.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana amehitimisha ziara yake ya kikazi ya Siku Mbili Mkoani Mwanza kwa kuzindua mradi wa Uboreshaji wa huduma ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika kijiji cha Nyamazugo Wilayani Sengerema.

Mradi huo wa maji umetekelezwa chini ya mpango wa maji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya shilingi bilioni 22.4. Mradi wa Maji Safi mjini Sengerema ulioanza tangu mwaka 2011 unatarajiwa kuwahudumia wakazi 138,000 ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi huo, Mhe. Rais Dkt. Magufuli amesema kukamilika kwa mradi huo kutamaliza tatizo la maji la muda mrefu kwa wakazi wa Sengerema na maeneo ya jirani.

Mhe. Rais Dkt. Magufuli amewataka wananchi wanaozunguka mradi huo kuutunza na kuhakikisha hawaharibu vyanzo vya maji katika eneo hilo la ziwa Victoria ikiwa ni pamoja na kuacha uvuvi haramu ambao umekuwa na madhara makubwa kwa wananchi.

Aidha, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mwanza na Vyombo vya Dola kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaochafua vyanzo vya maji katika eneo la Ziwa Victoria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *