Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari atakuwa kiongozi wa kwanza wa bara la Afrika kulakiwa na Rais wa Marekani Donald Trump White House atakapokutana na kiongozi huo kwa mashauriano rasmi mjini Washington baadaye leo.
Marais wengine wa Afrika wamewahi kukutana na Bw Trump akiwa rais, wakiwemo Paul Kagame wa Rwanda na Uhuru Kenyatta wa Kenya, lakini nje ya Marekani.
Rais Kenyatta alikutana na Trump pambizoni mwa mkutano wa G7 nchini Italia mwezi Mei mwaka jana, naye Rais Kagame akakutana na kiongozi huyo wa Marekani Januari mwaka huu mjini Davos, Uswizi pambizoni mwa mkutano mkuu kuhusu uchumi wa dunia.
Septemba mwaka jana, Rais wa Uganda Yoweri Museveni pia alikutana na kupigwa picha na Rais Trump kwenye dhifa iliyoandaliwa wakati wa mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa jijini New York. Hakukuwa na mazungumzo yoyote hata hivyo na haikuwa ziara ya kikazi kwa Bw Museveni.
Wawili hao wanatarajiwa kujadiliana kuhusu masuala ya kiuchumi na kiusalama watakapokutana leo.