Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amewapokea wasichana 106 na mvulana mmoja jijini Abuja.

Wasichana waliwasili mapema kwenye makazi ya Rais wakionekana wenye afya njema, isipokuwa wanne ambao wanaelezwa kuwa walivunjika miguu.

Wasichana walisafirishwa kwa ndege mpaka mjini Abuja siku ya Jumatano ambapo walitakiwa kwenda kufanya uchunguzi wa kitabibu na kiusalama baada ya kukabidhiwa kwa mamlaka za kiraia.

Buhari amewataka wasichana waendelee kutimiza ndoto zao bila kuogopa machafuko, amevitaka vyombo vya ulinzi kuhakikisha usalama unakuwepo kwenye shule zote zilizo hatarini kushambuliwa na kuonya kuwa iwapo tukio hilo litatokea tena hatalichukuliwa kirahisi.

Buhari amewataka wazazi ambao bado watoto wao wanashikiliwa kutokata tamaa wakati serikali yake inafanya jitihada kuwanasua.

Haijulikani kama kurejea kwao kwenye maisha ya kawaida ni suala la uchaguzi wakati huu ambao mustakabali wa elimu yao haujulikani, iliripotiwa kuwa wakati mabinti hao walipokuwa wakirejeshwa, wanamgambo walitoa tahadhari kuwa wasirejee tena shuleni.

Wakati hayo yakijiri Serikali ya Nigeria imesema haitapunguza jitihada zake za kumkomboa msichana mmoja aliyebaki mikononi mwa Boko Haram baada ya kutekwa mjini Daptchi mwezi uliopita.

Msichana huyo ni miongoni mwa wasichana 110 waliochukuliwa wakiwa shuleni, wanamgambo walipovamia mji tarehe 19 mwezi Februari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *