Rais wa Gabon, Ali Bongo amesema yuko tayari kutii uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba iwapo mahakama hiyo itaagiza kura za uchaguzi mkuu uliofanyika wiki mbili zilizopita zihesabiwe upya.

Waangalizi wa kimataifa wamesema kuna kasoro nyingi kwenye matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa, ambayo yalimpa Bw Bongo ushindi mwembamba.

Bongo amesema sheria za nchi zake haziruhusu kura zihesabiwe tena lakini atakubali hilo iwapo mahakama itaamua hilo lifanyike.

Mahakama ya kikatiba inatarajiwa kukutana kesho kuangazia kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo ambayo iliwasilishwa na mgombea wa upinzani, Jean Ping.

Bongo amesema suala kuu kwake kwa sasa ni kurejesha utulivu nchini humo na kuiwezesha Mahakama ya Kikatiba ifanye kazi yake.

Ali Bongo alitangazwa mshindi wa uchaguzi lakini upinzani ukiongozwa na Jean Ping ulipinga matokeo.

Bongo alipata 49.8% ya kura naye Bw Ping akiwa na 48.2%, tofauti kati yao ikiwa kura 5,594.

Bw Ping alishinda majimbo sita kati ya tisa na ameomba kurudiwa tena kwa shughuli ya hesabu ya kura.

Katika jimbo la Haut-Ogooue, anamotoka Bw Bongo, waliojitokeza kupiga kura walikuwa 99.93% kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na 95% ya kura zilimpigia rais huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *