Mgombea urais kupitia muungano wa upinzani (NASA) nchini Kenya, Raila Odinga amepinga matokeo ya uchaguzi ambayo yanaendelea kutangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo, IEBC.

Odinga amewaambia wanahabari kwamba tume hiyo imekuwa ikitangaza matokeo kwenye tovuti yake bila kufuata utaratibu unaofaa.

Waziri mkuu huyo wa zamani amesema kabla ya matokeo yoyote kutangazwa, IEBC inafaa kuwapa maajenti wa vyama Fomu 34A kutoka vituoni.

Amesema kwa sasa, bila kuwepo kwa fomu hizo, ni vigumu kubaini matokeo yanayopeperushwa yanatoka wapi.

IEBC imekuwa ikitangaza matokeo ya urais mtandaoni, na kufikia saa tisa na robo alfajiri, matokeo hayo yalikuwa yanamuonyesha Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee akiwa mbele na kura 6331140 (55.27%) naye Bw Odinga akiwa na kura 5031737 (43.92%).

Matokeo hayo ni ya kutoka vituo 295319 kati ya vituo 40883 nchini humo ambapo hadi sasa yanaendelea kutangazwa.

Hali ya wasiwasi imekuwa ikitanda katika kituo cha taifa cha kujumlishia na kutangaza matokeo katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi.

Matokeo yalianza kutangazwa jana baadaye jioni baada ya shughuli ya kuhesabiwa kura kuanza. Matokeo hayo yamekuwa yakionesha Bw Kenyatta akiongoza.

Wakala mkuu wa muungano huo wa upinzani, naibu waziri mkuu wa zamani Musalia Mudavadi alikuwa awali amehutubia wanahabari na kutaja matokeo yanayotangazwa na tume hiyo kama utapeli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *