Takriban raia 90 wa Somalia na wawili wa Kenya wametimuliwa kutoka Marekani saa chache baada ya taarifa kuibuka kwamba Rais Donald Trump atakabiliana na watu wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria.

Wote wamewasili katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi nchini Kenya walipofikia.

Msemaji wa serikali ya Kenya Eric Kiraithe amesema kwamba raia hao wa Somalia watasafirishwa moja kwa moja hadi Mogadishu.

Kuhusu sababu iliyowafanya kufurushwa, Bw Kiraithe amesema: “Inategemea sheria za nchi ambayo walikuwa wamehamia (Marekani),”.

Bw Trump alisema Jumatano itakuwa siku muhimu kwa usalama wa Marekani.

Anatarajiwa kuweka masharti makali kwa raia wa mataifa saba ya Mashariki ya Kati na Afrika yenye idadi kubwa ya Waislamu wanaotafuta viza za kwenda Marekani.

Taarifa zinasema nchi hizo ni Syria, Iraq, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *