Mwanamuziki wa Marekani, R Kelly ameachiwa huru kutoka gerezani Chicago Marekani baada ya kulipa dhamana ya $100,000.
Mapema Jumatatu alikana mashtaka 10 ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake wanne, watatu kati yao walikuwa ni watoto wakati wa uhalifu huo.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 52 alionekana akiwa amevaa koti la samawati, hakuzungumza na waandishi habari aliposindikizwa kutoka gerezani na wakili wake.
Msemaji wa idara ya polisi Sophia Ansari amethibitisha Jumatatu kwamba R Kelly amelipa dhamana hiyo ya $100,000 ambayo ni 10% ya dhamana ya dola milioni moja iliyowekwa na jaji mwishoni mwa juma.
Kufika kwake mahakamani na kukana mashtaka hayo kunajiri wiki kadhaa baada ya makala ndefu kwa jina ‘Suriving R Kelly kupeperushwa. Ilituhumu unyanyasaji dhidi ya wanawake wengi, akiwemo aliyekuwa mkewe nyota huyo muimbaji.
Alikutana na mojawapo ya wanawake hao aliyekuwa anaadhimisha miaka 16 tangu kuzaliwa katika mgahawa mmoja – na mwingine ambaye pia alikuwa na umri wa miaka 16 – aliyeomba amtilie saini nakala ya kazi yake – au autograph.
Mahakama imemuagiza muimbaji huyo ambaye jina lake halisi ni Robert Sylvester Kelly, asalimishe pasi yake ya usafiri na asiwasiliane na mtu yoyote aliye na umri wa chini ya miaka 18.
Inaarifiwa kwamba alipata tabu kulpa dhamana hiyo ya $100,000 iliyohitajika kutoka katika gereza la Cook County Jail.
Katika mkutano na waandishi habari baadaye, wakili maarufu Gloria Allred amesema kwamba sasa anawawakilisha wanawake sita wanaotuhumu kuwa muimbaji huyo aliwanyanyasa.