Waziri wa Afya wa eneo la Gauteng, nchini Afrika Kusini, Qedani Mahlangu, amejiuzuru kazi kufuatia ripoti ya vifo vya wagonjwa wa akili 94 vilivyotokea kwenye jimbo la Gauteng mwaka jana.

Ripoti hiyo ya mchunguzi wa malalamiko katika sekta ya afya imedai kuwa wagonjwa wengi ambao gharama zao za matibabu zinalipwa na jimbo la Gauteng walikufa kwa maradhi ya kuharisha, upungufu wa maji mwilini na njaa.

Mtoa ripoti hiyo, Dk. Malegapuru Makgoba amesema kuwa vifo hivyo vilitokea kati ya mwezi Machi na Disemba mwaka jana wakati wagonjwa 1,900 walipohamishwa kutoka kituo cha afya chenye leseni ya kuwahudumia wagonjwa hao cha Life Esidimeni kwenda kwenye taasisi 27 zisizo za kiserikali ambazo hazikuwa na leseni halali za kuwauguza wagonjwa wa akili.

Dk. Makgoba amesema kuwa idara ya afya ya jimbo la Gauteng ilifanya uzembe na ilipuuzia hatari iliyokuwa ikiwakabili wagonjwa hao ilipoharakisha kuwahamisha wagonjwa kwa lengo la kuokoa pesa.

‘Hivyo wagonjwa walikufa kinyume cha sheria’. 

Idara ya afya ya Gauteng siku zote imekuwa ikidai kuwa waliofariki ni 36.

Dk. Makgoba amesema kuwa wakati Bi. Mahlangu alipotangaza hadharani kwenye bunge la Gauteng kuwa waliofariki ni 36, tayari wagonjwa 77 walikuwa wameshafariki.

Ripoti hiyo iliyopewa jina la ‘94 Silent Deaths and Counting’ imesema kuwa ni mgonjwa mmoja tu ndiye aliyefariki kutokana na maradhi ya akili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *