Rais wa Urusi, Vladimir Putin amesema mazungumzo ya kusitisha mapigano nchini Syria yaliyofanyika Astana mwaka huu yamesaidia kufungua njia ya mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

Awamu ya kwanza ya ya mazungumzo katika mji mkuu wa Khazakhstan, Astana yaliyofanyika mnamo mwezi Januari, Urusi na Iran ambao ni washirika wa Rais wa Syria, Bashar al-Assad na Uturuki ambaye ni mpinzani wa Assad, kwa pamoja walitiliana saini makubaliano tete ya kusitisha mapigano kati ya waasi na serikali ya Syria.

Putin alinukuliwa akiwaambia waandishi wa habari alipofanya ziara nchini Khazakhstan kwamba “utaratibu  wa kusimamia mpango huo wa kusitisha mapigano umekwishaandaliwa, na hilo ndilo suala muhimu zaidi”. Aliongeza kuwa huu ndio msingi uliofungua ukurasa wa kuanza upya kwa mazungumzo mjini Geneva.

Makubaliano yaliyofikiwa Astana ya kusitisha mapigano yamekuwa yakivunjwa mara kwa mara, wakati ambapo vita dhidi ya makundi ya Jihadi, ambayo ni pamoja na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, ambalo halikuuhusishwa kwenye mpango huo huku vita vikiendelea kusambaa.

Hapo jana mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura alikutana na makundi mawili ya upinzani yanayoungwa mkono na Urusi, ambaye ni mshirika mkubwa wa Rais Assad.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *