Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi kutunza na kuilinda miundombinu ya barabara na kuwaonya wale wote watakaohusika kuihujumu na kuiharibu, watashughulikiwa.
Profesa Makame Mbarawa amesema hayo wakati akikagua ujenzi wa barabara za Sakina – Tengeru yenye urefu wa kilometa 14.1 na Southern bypass yenye urefu wa kilometa 42.5 ambazo kwa pamoja zimegharimu kiasi cha Sh bilioni 132.3.
Profesa Mbarawa alipotembelea barabara ya kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) hadi Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara yenye urefu wa kilometa 27, alisema serikali imetumia fedha zake za mapato ya ndani kiasi cha Sh bilioni 32.2.
Amesema serikali inatumia gharama kubwa kujenga barabara hizo ili zisaidie kurahisisha shughuli za kila siku za maendeleo na kuharakisha kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa kila mwananchi anao wajibu wa kuzilinda barabara na madaraja na kuyatunza kwa kujali alama na mipaka yake.
Akizungumza katika Mji wa Mirerani, Profesa Mbarawa alisema pamoja na eneo hilo kuwa na madini ya vito, lakini tangu dunia iumbwe hawakuwahi kupata barabara ya lami, lakini Serikali ya Awamu ya Tano imewajengea na iko karibu kukamilika.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Arusha, Mgeni Mwanga aliwataka wananchi waendelee kuwa wavumilivu wakati miradi hiyo ikiendelea hasa pale kunapojitokeza changamoto mbalimbali ikiwemo kuzifunga barabara kwa muda.