Mtayarishaji wa muziki wa Bongo Fleva, P Funk Majani amemaliza tofauti iliyokuwepo kati yake na Mbunge wa jimbo la Mikumi ambaye pia ni mwanamuziki wa Bongo Fleva, Prof Jay.
Picha hiyo imepostiwa katika mtandao wa Twitter na Instagram za akaunti ya Prof Jay baada ya kutembelewa na P Funk Majani na msanii Mwana Fa katika studio yake mpya ya Mwanalizombe iliyopo Mikumi mkoani Morogoro.
“Ni baraka juu ya baraka mwanalizombe studios inazidi kupasua anga “Bomb Bomb Fire” na leo tumebahatika kutembelewa na magwiji wawili P Funk Majani na Mwana Fa, yaliyopita si ndwele tumeamua kuganga yajayo, tumerudi kufanya kazi pamoja tukiwa imara zaidi, yajayo yanafurahisha , eeeh Mwenyezi Mungu tusaidie”.
Mashabiki na Baadhi ya mastaa mbalimbali walionekana kufurahia kuona wawili hao kuungana pamoja huku wengine wakisema hiyo ni picha bora ya mwezi Julai.
Ukaribu wao uliingia tofauti baada ya P Funk Majani kupokea Milioni 100 za haki miliki za wimbo alioutengeneza ambao uliotumiwa na msanii wa Uganda, ambapo Cosota walidai kwamba pesa hizo alilipwa Prof Jay.