Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole Gabriel amewaaga watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo leo mjini Dodoma.

Prof. Elisante awali ndiye alikuwa anaiongoza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kabla ya mabadiliko ya safu ya Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli hapo jana.

Prof. Elisante amewashukuru watumishi hao kwa ushirikiano waliompatia tangu alipoingia Wizarani hapo Aprili 01, 2012 akiwa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana, Naibu Katibu Mkuu na baadae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

Aidha, amewataka watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa wabunifu ili utendaji kazi wao uwe wenye tija kwa wananchi wote watakao kuja kupata huduma wizarani hapo.

Kwa upande wa watumishi wa Wizara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Maedeleo ya Utamaduni Bi. Lilly Beleko amemhakikishia Prof. Elisante kuwa wataendelea kutumia fursa zilizopo kwa maedeleo ya Wizara na taifa kwa ujumla kwa kutumia ujuzi walionao kulingana na taaluma zao.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo sasa inaongozwa na viongozi wapya ambapo Katibu Mkuu wake ni Bi. Suzan Paul Mlawi na Naibu Katibu Mkuu akiwa Nicholaus B. William.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *