Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam, Simon Sirro amesema jeshi hilo limemkamata mtuhumiwa ‘Scorpion’ aliyehusika katika matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha eneo la Buguruni jijini humo.
Sirro alitoa kauli hiyo jana Buguruni kwa Mnyamani jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kujadili usalama katika eneo hilo ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Amesema mtuhumiwa huyo anayejulikana kwa jina maarufu kama Scorpion alikamatwa baada ya polisi kupewa taarifa za matukio ambayo ameyafanya ikiwemo la kumchoma kisu, kumtoa macho na kumsababishia upofu, Said Ally.
Aidha Sirro amesema baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo na kuhojiwa aliutaja mtandao wake wote na tayari wameukamata, hivyo amewataka wakazi wa eneo hilo kutokuwa na hofu kwani mtuhumiwa huyo hayupo tena katika eneo hilo..
Kabla ya kauli hiyo ya Sirro, wananchi wamelalamikia askari wa eneo hilo ambao walishindwa kuchukua hatua kwa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akifahamika muda mrefu.
Sadiki Mgaya ambaye alishuhudia tukio la kuchomwa kisu na kutolewa macho kwa Said Ally, alisema mtuhumiwa huyo alisema kuwa amekuja kwa ajili ya kulipa kisasi kwa wakabaji baada ya yeye kukabwa.
Amesema baada ya kufanya tukio hilo, askari walifika katika eneo hilo na mtuhumiwa huyo akiwa hapo na wananchi waliwaonesha askari lakini hawakuchukua hatua zozote badala yake waliwataka wananchi wamkamate.
Aidha wananchi hao pia wamemlalamikia Mkuu wa Kituo cha Polisi Mnyamani na kudai kuwa amekuwa akipelekewa taarifa za uhalifu ikiwemo za vibaka lakini mtu anapokamatwa akifika kituoni hapo anatoa rushwa na kuruhusiwa kuondoka.
Kauli hizo za wananchi zikamfanya Sirro kutoa kauli ambapo amesema askari na maofisa wote ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao watachukuliwa hatua ikiwemo kufikishwa mahakamani pamoja na kufukuzwa kazi.