Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imefanya operesheni katika maeneo ya katikati na pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam na kuwakamata watuhumiwa 87 wa makosa mbalimbali, wakiwemo waliokuwa kwenye mtandao wa uhalifu wa mkazi wa Machimbo Yombo jijini Dar es Salaam, Salum Njwele (34) maarufu kama ‘Scorpion’.

Njwele alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mwishoni mwa wiki, kujibu mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kumtoboa macho yote mawili Said Mrisho.

Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi Simon Sirro alisema watuhumiwa wengine wanadaiwa kuvunja nyumba na kuiba na wengine walipatikana na gongo lita 148, bangi kete 95 na puli 48.

Amesema watuhumiwa hao, wamekamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Mbagala, Buguruni, Kiluvya, Gongo la Mboto, Tandika, Ukonga, Banana, Kunduchi, Keko, Kawe.

Katika tukio lingine, watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamekamatwa wakiwa na silaha aina ya MARK IV ikiwa imekatwa kitako chake.

Watuhumiwa hao walikamatwa Oktoba 10 mwaka huu saa 3:30 asubuhi huko maeneo ya Vingunguti wakiwa na pikipiki yenye namba MC 787 BEP aina ya Boxer ikiwa kwenye jaribio la kufanya tukio la ujambazi katika eneo la viwandani.

Amesema Kikosi Maalumu cha Kupambana na ujambazi wa kutumia silaha kiliwafuatilia na watuhumiwa hao baada ya kuona hivyo walianza kufyatua risasi hovyo kuelekea kwa askari na ndipo askari walijibu mashambulizi na kuwajeruhi wote wawili na kuchukua silaha hiyo, ikiwa na risasi tano kwenye magazine moja tayari kwa kufyatuliwa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *