Wanamgambo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamewashambulia na kuwaua kwa kuwakatakata wanajeshi takriban 40 baada ya kuwavizia katika mkoa wa Kasai, katikati mwa nchi hiyo.
Wapiganaji kutoka kundi la Kamwina Nsapu walishambulia polisi waliokuwa kwenye msafara nchini humo.
Maafisa sita wa Polisi waliowasiliana na Tshiluba waliachiliwa huru, rais wa bunge la jimbo la Kasai Francois Kalamba amesema.
Machafuko jimbo la Kasai yalianza Agosti mwaka jana, pale maafisa wa polisi walipomuua kiongozi wa Kamwina Nsapu.
Shambulio la Ijumaa lililenga msafara wa polisi waliokuiwa wakisafiri kati ya Tshikapa na Kananga.
Gavana wa jimbo hilo Alexis Nkande Myopompa amesema uchunguzi umeanzishwa kuhusu mauaji hayo.
Umoja wa Mataifa unasema watu 400 wameuawa na wengine 200,000 kuachwa bila makao eneo la Kasai tangu Jean-Pierre Pandi, kiongozi wa Kamwina Nsapu alipouawa.
Mauaji yake yalitekelezwa miezi miwili baada ya Kamwina Nsapu mwezi Juni 2016 kuanzisha juhudi za kutaka atambuliwe kama mkuu wa eneo hilo na kutaka maafisa wa serikali ya taifa kuondoka jimbo hilo.