Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole amesema viongozi wa vyama vya upinzani wanaodai kuwa wamenyamazishwa ni waongo na wanafiki na wanapaswa kuupuzwa kwa kuwa sio wakwelI.
Polepole amesema kazi ya siasa si kupiga domo bali kufanya kazi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo ya wananchi, hivyo wanaodhani kuwa kazi hiyo ni kupiga domo watafakari vizuri.
Ameyasema hayo katika mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Twaweza wa kujadili mambo yanayoendelea kwa sasa nchini pamoja na kujadili ripoti ya Sauti za Wananchi iliyotolewa na Twaweza.
“Hawa wanasiasa uchwara wakati mwingine tuwapuuze, kwanini hawaandamani katika baadhi ya maeneo, kwanini hawaandamani kule Moshi, kwanini hawaandamani kule Kigoma, badala yake wanataka kuandamana katika maeneo yale ambayo CCM tumejikita katika maendeleo ya wananchi,” amesema.
Ameongeza kuwa ni vyema wanasiasa wanaodai kuwa wamefungwa mdomo na kuzuiwa kuandamana waanze kuandamana katika maeneo yao kwa kufuata taratibu kisha ndio walalamike kuwa wananyimwa kufanya siasa.