Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm ameikubali Mbeya City na kusema ni timu nzuri yenye uwezo wa kucheza dakika 90 kwa ushindani.
Aidha kocha huyo amelaumu wachezaji wake kutokuwa makini mwanzoni mwa mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City kwa kuruhusu kufungwa bao la mapema.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Yanga ililala kwa mabao 2-1.
Pamoja na malalamiko hayo kwa wachezaji wake, Pluijm amemlaumu mwamuzi Rajab Mrope wa Ruvuma kuwa ndio amewanyonga katika mchezo huo.
Pluijm amesema kuwa bao la pili katika mchezo huo halikustahili kwani maamuzi yake yalikuwa na utata na kwamba aliwaamuru wachezaji wake warudi nyuma kabla ya filimbi kupigwa na Mbeya City wakatumia mwanya huo kufunga.
Kwa matokeo hayo, Yanga ambao ni mabingwa watetezi wanabaki na pointi zao 27 wakiwa wamecheza mechi 13 wakiwa nyuma ya pointi nane dhidi ya mahasimu wao Simba ambao wana pointi 35 wakicheza michezo 13 sawa na Yanga.