Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm amesema presha waliyokuwa nayo wachezaji wake katika mechi dhidi ya Azam ndio chanzo cha kukosa matokeo mazuri.

Yanga na Azam zilikutana katika mechi ya Ligi Kuu mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Uhuru na kutoka suluhu.

Kocha huyo amesema kila upande ulikuwa na presha katika mechi hiyo kwani timu zote zilihitaji matokeo mazuri kutokana na kufanya vibaya katika mechi zake.

Matokeo ya juzi yaliifanya Yanga kubaki kwenye nafasi ya tatu ikiwa na pointi 15 na Azam ikiwa nafasi ya 10 baada ya kufikisha pointi 12.

Simba ndio inaongoza ligi kwa kuwa na pointi 23 na Majimaji inashika mkia ikiwa na pointi sita.

Pluijm amesema kikosi chake kilicheza vizuri kipindi cha kwanza na kutengeneza nafasi karibu nne lakini walishindwa kuzitumia na kwamba Azam FC iliwazidi kipindi cha pili kwani nao walicheza vizuri na kutengeneza nafasi walizoshindwa kuzitumia.

Pluijm amesema wataendelea kujipanga kwa michezo ijayo kuhakikisha wanafanya vizuri. Yanga inatarajiwa kusafiri leo kwa ndege kuelekea Mwanza ambapo itakuwa na mchezo dhidi ya Toto Africans keshokutwa kabla ya kucheza na Kagera Sugar wiki ijayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *