Kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Italia Andrea Pirlo ametangaza kustaafu soka baada ya kuchez mechi yake ya mwisho klabu ya New York City.
Mchezaji huyo mwenye miaka 38 alichezea Italia mechi 116 na aliwasaidia kushinda Kombe la Dunia mwaka 2006.
Pirlo alianza uchezaji wake Brescia na alichezea Inter, AC Milan na Juventus kabla ya kujiunga na Ligi Kuu ya Soka Amerika Kaskazini (MLS) miaka miwili iliyopita.
Pamoja na kuwasaidia Azzurri kuwa mabingwa wa dunia, Pirlo alishinda mataji mengi ya soka nchini mwake katika miaka 22 aliyocheza soka.
Alikuwa kwenye kikosi cha Milan kilichoshinda mataji mawili ya Serie A, vikombe viwili vya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na Kombe la Dunia la Klabu kati ya 2003 na 2011, na kisha akachangia sana ushindi wa Juventus wa ligi mara nne kati ya 2012 na 2015.
Alihamia New York kabla ya kuanza kwa msimu wa MLS wa mwaka 2015 na kujiunga na kiungo wa kati wa zamani wa England Frank Lampard ana mshambuliaji wa zamani wa Uhispania David Villa katika klabu hiyo inayomilikiwa na Manchester City.
Alisaidia klabu hiyo ambayo mkufunzi wake ni Patrick Vieira kufika mechi za muondoano kutafuta bingwa misimu miwili iliyopita, lakini hakuweza kushinda vikombe akiwa nao.