Mchekeshaji wa kundi la Orijino Komedi, Lucas Mhuvile maarufu kwa jina la Joti mwisho wa wiki iliyopita alifunga ndoa na mpenzi wake wa siku nyingi aitwae Tumaini Salehe.

Harusi ya msanii huyo imefanyika siku ya jumamosi katika Kanisa Katoliki lililopo Magomeni jijini Dar es Salaam.

Kilichowashangaza watu kwenye harusi hiyo ni staili ya nywele ya Joti ambapo amenyoa mtindo wa kuacha nywele katikati ya kichwa maarufu kama ‘kiduku’ na kuingia ndani ya kanisa bila wasi wasi wowote.

Kitendo hicho kiliwafanya baadhi ya waumini waliojazana ukumbini hapo kupigwa na butwaa. “Sasa hivi ndiyo nini tena jamani? Yaani kweli padri anaruhusu hili jambo linafanyika kanisani?

Huu si mtindo wa vijana wa kihuni wanaouonesha huko mitaani, unaruhusu hili jambo au kwa sababu huyu ni kijana maarufu?” Alihoji mama mmoja aliyekuwepo kanisani hapo siku ya harusi hiyo.

Muumini mwingine ambaye naye alikuwepo kanisani hapo, alisema kuwa, kitendo cha kuruhusu watu kuoa wakiwa na nywele za mitindo ya kihuni kama vile siyo sawa, kwani ni rahisi kuruhusu vitu vingine visivyo vya kimaadili kufanywa na vijana hasa wa kizazi cha sasa.

Kwa upande wa padri wa kanisha hilo Father Paul Sabuni amesema kuwa kiduku hakijawahi kuwa tatizo kwa Kanisa Katoliki.

Padri huyo amesema kuwa “Kanisa haliangalii mavazi au namna mtu alivyo, kanisa linaangalia moyo wa mtu, kama roho yake iko safi hicho ndicho tunachokitaka, suala la kiduku halina nafasi kwetu, tunashughulika na imani yake, si muonekano wala mavazi yake, hao wanaofikiri hivyo wanapaswa kupewa somo.

 Joti anakuwa msanii wa pili wa kundi la Olijino Komedi kufunga ndoa baada ya muigizaji mwenzake Masanja Mkandamizaji kufunga ndoa mwaka jana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *