Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemchagua Mhe. Naghenjwa Kaboyoka Mbunge wa Same Mashariki (Chadema) kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

 

Tangu kuundwa kwa Kamati hiyo ambayo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge inatakiwa kuongozwa na Upinzani ilikuwa bado haijamchagua Mwenyekiti na hivyo ilikuwa chini ya Uongozi wa Makamu Mwenyekiti Mhe. Aeshi Hilaly (Mb).

 

Katika uchaguzi huo Mhe. Kaboyoka hakupigiwa kura badala yake alipendekezwa na Wajumbe wa Kamati hiyo ambapo wote waliridhia awe Mwenyekiti wao.

 

Kamati hiyo ilikutana katika kikao chake cha kwanza chini ya Mwenyekiti Mhe. Kaboyoka ambapo mara baada ya kufanya uchaguzi huo ilijadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Hoja za Ukaguzi kwa Mashirika yaliyoko chini ya SUMA JKT.

 

Wajumbe wa Kamati hiyo walisema hesabu za mashirika hayo hazijazingatia sheria na utayarishaji wa hesabu na kwamba matumizi yao yamezidi bajeti iliyoidhinishwa.

Kamati hiyo ilitoa ushauri kwa SUMA JKT kuhakikisha wanaajiri wahasibu wenye ujuzi badala ya kuajiri watu ambao hawana ujuzi wa kuandaa taarifa za fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *