Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema baada ya uchambuzi wa maombi ya mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2017/2018, orodha ya awamu ya kwanza yenye wanafunzi 10,196 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo imekamilika.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo amesema Sh34.6 bilioni zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi hao 10,196.
Amesema kwa jumla Sh108.8 bilioni zitatolewa kwa wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2017/2018.
Badru amesema orodha ya awamu ya kwanza inapatikana kwenye tovuti ya Bodi ya Mikopo http://www.heslb.go.tz/ na itatumwa kwa vyuo husika.
Amesema orodha nyingine (batches) zitafuata kwa kadri utaratibu wa udahili na uchambuzi unavyokamilika.
Mkurugenzi mtendaji huyo amesema orodha hiyo ya wanafunzi 10,196 imepatikana baada ya kupokea na kuchambua awamu ya kwanza ya majina ya wanafunzi 32,495 waliopata udahili katika chuo kimoja.
Amesema wanafunzi waliopata udahili katika chuo zaidi ya kimoja na ambao wana sifa za kupata mikopo, watapangiwa mikopo baada ya kuchagua na kuthibitisha chuo watakachojiunga kwa ajili ya masomo.
Pia Badru amesema wanatarajia kuanza kutuma vyuoni fedha za mikopo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao wamefaulu mitihani yao kuanzia leo Jumatano, Oktoba 18, 2017.
Amesema Sh318.6 bilioni zitatolewa kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo kwa mwaka 2017/2018.
Bodi imewasihi waombaji wa mikopo kuwa na subira wakati ikiendelea kukamilisha maandalizi ya orodha zinazofuata za wanafunzi waliopata mikopo.