Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amempongeza Edward Lowassa baada ya kupongeza hatua ya Rais John Pombe Magufuli kuhusu mchanga wa madini yanayochimbwa nchini na kampuni ya Acacia.
Ole Sendeka amesema kuwa baada ya kusikia kupitia vyombo vya habari kuwa Lowassa amempongeza Rais, hana budi kumshukuru na kumpongeza pia kwa kufanya hivyo.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Njombe alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza jana kwenye mazishi ya mama yake mzazi yaliyofanyika katika kijiji cha Losokonoi wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Pia alimuomba mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya ambaye alihudhuria mazishi hayo, kumfikishia salamu na pongezi hizo kwa Lowassa.
Lowassa alimpongeza Rais Magufuli kwa uamuzi wake baada ya kupokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa makontena ya mchanga wa madini yanayoshikiliwa na Serikali katika bandari ya Dar es Salaam, yalipokuwa katika mchakato wa kusafirishwa nje ya nchi na kampuni ya Acacia.