Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga amewaambia wafuasi wake wasitishe kampeni ya kususia bidhaa na biashara za kampuni zilizohusishwa kuwa na uhusiano na chama tawala nchini Jubilee cha rais Uhuru Kenyatta.
Safaricom, kampuni kubwa ya mawasiliano ya simu nchini na Brookside, ambayo ni kampuni ya kutengeneza bidhaa kama maziwa na siagi nimiongoni mwa kampuni zilizolengwa.
Mnamo mwezi Machi mwaka huu kiongozi huyo mkongwe wa kisiasa Kenya alipatana na rais Uhuru Kenyatta na viongozi hao wawili kwa sasa wanashirkiana katika ‘kujenga madaraja’.
Tangazo hilo la kususia bidhaa za wanaotajwa kuwa washirika wa chama tawala lilitolewa mnamo Novemba mwaka jana baada ya uchaguzi mkuu uliokumbwa na mzozo ulioshuhudia Kenya kuwa nchi ya kwanza Afrika na ye nne pekee duniani kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais.
Raila Odinga amesema maafikiano yake na Uhuru Kenyatta yalioidhinishwa kwa kusalimiana kwa mikono viongozi hao wawili mnamo Machi 9, yamechangia amani na kuruhusu Wakenya kuendelea.
Tangazo la leo litaonekana kama mfano mwingine wa kupatana na kurudi kwa uhusiano mwema baina ya viongozi wawili.